BBC Russian
Svoboda | Graniru | BBC Russia | Golosameriki | Facebook
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo
Matangazo
Matangazo

Habari

Habari za Ulimwengu | 12.10.2020 | 15:00

Makabiliano kati ya Amernia, Azerbaijan yatishia usitishaji uhasama

Mpango wa kusitisha mapigano kati ya Armenia na Azerbaijan kuhusu mkoa unaozozaniwa wa Nagorno-Karabakh yameonekana kushindwa leo, wakati ambapo mataifa hayo mawili yakishambuliana upya huku wapatanishi wa kimataifa wakitarajiwa kuanzisha juhudi mpya za mapatano endelevu. Urusi imezitaka pande hizo mbili kuuheshimu mpango huo wa kuweka chini silaha. Armenia na Azerbaijan zimeshirika mapambano makali kwa wiki mbili sasa, kuwania udhibiti wa eneo la Nagorno-Karabakh, ambao ni mkoa uliojitenga na Azerbaijan na unaodhibitiwa na Warmenia baada ya vita vya 1994 na ambao bado unatambuliwa kimataifa kama sehemu ya Azerbaijan. Mapigano hayo ambayo ndiyo mabaya zaidi tangu usitishaji mapigano wa mwaka 1994, yamezusha hofu ya mzozo wa kikanda, ambapo Uturuki umeiunga mkono wazi Azerbaijan, huku Armeni ikitafu kuivutia mshirika wa zamani wa Kisoviet Urusi upande wake, na Iran ikifuatilia mzozo huo kwa wasiwasi.

Mvutano wa Ugiriki-Uturuki waongezeka kuhusu mashariki mwa Mediterania

Meli ya utafiti ya Kituruki imeelekea leo mashariki mwa bahari ya Mediterania, hatua iliyoifanya Ugiriki kutoa takwa kali la vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Ankara katika mzozo kuhusu haki za uchimbaji mafuta na gesi baharini. Ufaransa imeelezea wasiwasi wake baada ya meli hiyo ya Uturuki, kwa jina Oruc Reis kung'oa nanga. Imesema Uturuki lazima iheshimu ahadi ilizotoa katika mgogoro huo, kujizuia na vitendo vya uchochezi na kuonyesha nia njema. Wizara ya mambo ya kigeni ya Ugiriki imeielezea safari hiyo mpya kuwa hatua ya kuongeza mvutano na kitisho cha moja kwa moja kwa amani ya kikanda. Uturuki inaituhumu Ugiriki kwa kuongeza mvutano. Meli ya Oruc Reis inanuia kufanya kazi ya utafiti kusini mwa kisiwa cha Ugiriki cha Kastellorizo, ambacho kipo karibu na pwani ya Uturuki.

EU kutangaza vikwazo vipya dhidi ya Urusi kuhusu kupewa sumu Navalny

Umoja wa Ulaya umeorodhesha vikwazo dhidi ya maafisa wa Urusi kuhusiana na kupewa sumu kiongozi wa upinzani Alexei Navalny na dhidi ya kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko kuhusiana na mzozo wa kisiasa nchini mwake. Mawaziri wa mambo ya kigeni wanaokutana mjini Luxembourg wamekubaliana kimsingi kuhusu mapendekezo ya vikwazo vilivyotayarishwa na Ufaransa na Ujerumani wiki iliyopita, ambayo yalisema Urusi ilihusika na tukio la Navalny kupewa sumu inayoathiri mishipa ya fahamu aina ya Novichok. Kuhusu Belarus, mawaziri hao wamesema wako tayari kumuwekea vikwazo kiongozi wa nchi huyo Lukashenko, wakati umoja huo ukilenga kuongeza mbinyo kwa ukandamizaji unaofanywa na utawala wake dhidi ya waandamanaji. Umoja wa Ulaya tayari umeweka vikwazo vya kusafiri na kuzuwia mali za washirika 40 wa Lukashenko kwa wizi wa kura katika uchaguzi wa Agosti ambao ulimrejesha madarakani na kisha akaamuru ukandamizaji dhidi ya maandamano ambayo yameikumba nchi hiyo tangu uchaguzi huo.

Taliban yafanya mashambulizi makubwa Helmand

Maafisa nchini Afghanistan wamesema wapiganaji wa kundi la Taliban wamefanya mashambulizi makubwa nje ya mji mkuu wa mkoa wa kusini wa Helmand. Tangu kuanza kwa mashambulizi hayo siku ya Ijumaa, wapiaganaji wameweza kuiteka wilaya ya nne ya kipolisi iliyoko umbali wa kilomita 16 kutoka katikati mwa mji wa Lashkargah. Mapigano makali yalikuwa yanaendelea kwingineko nje ya mji huo, kulingana na msemaji wa gavana wa mkoa Omar Zwak na diwani Hayatullah Mayar, waliozungumza na shirika la habari la Ujerumani dpa. Mapigano hayo yanakuja wakati timu kutoka serikali ya Afghanistan na Taliba zikishindwa kupiga hatua tangu kuanza kwa mazungumzo ya amani katikakati mwa Septemba mjini Doha, nchini Qatar. Mapigano hayo mapya yameripoti kusababisha vifo vya wanajeshi na raia, lakini idadi halisi haijajulikana. Maafisa wamesema familia kadhaa, zikiwemo za baadhi ya viongozi wa kikabila wanaoiunga mkono serikali na maafisa wa polisi zimeyakimbia maakazi yao kuepuka mapigano. Taliban hata hivyo haijazungumzia mapigano hayo. Rais Ashraf Ghani amsema katika mazungumzo ya simu na gavana wa Helmand kwamba mashambulizi ya maadui dhidi ya mkoa huo yatawagharimu sana.

Polisi ya Belarus kutumia silaha za moto dhidi ya waandamanaji

Polisi nchini Belarus sasa wataruhusiwa kutumia silaha za kivita mitaani kama kutakuwa na haja ya kufanya hivyo ili kukabiliana na kile wizara ya mambo ya ndani imeelezea kuwa ni kuongezeka kwa maandamano makubwa ya msimamo mkali dhidi ya serikali. Wizara hiyo imesema maandamano hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yamehamia katika mji mkuu Minsk, yamekuwa ya kupangwa na ya hisia kali. Polisi imesema imewakamata watu 713 katika maandamano ya jana ambapo vikosi vya usalama vilitumia mizinga ya maji na virungu kuyavunja makundi yanayodai uchaguzi mpya wa rais. Maelfu ya Wabelarus wameandamana kila mwisho wa wiki tangu uchaguzi wa Agosti 9 ambao Rais Alexander Lukashenko alitangazwa mshindi. Wapinzani wake wanadai matokeo yalichakachuliwa, Lukashenko anakanusha kuiba kura. Viongozi wengi wa upinzani wamekimbia nchini au kukamatwa.

Hariri kukutana na vyama vya kisiasa Lebanon kuhusu mpango wa Ufaransa

Waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Saad Hariri ambaye anatafuta muhula mpya, amesema atakutana na vyama vyote muhimu ili kutathmini dhamira yao ya kuutekeleza mpango wa uokozi uliopendekezwa na Ufaransa. Nchi hiyo imekuwa muflisi, lakini tabaka la watawala mpaka sasa limeshindwa kuitikia miito ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wa kuunda haraka serikali huru. Hariri ambaye mwenyewe ni mmoja wa vogogo wa jadi waliorithi siasa za Lebanon, alijiuzulu kutoka wadhifa wa waziri mkuu mwaka mmoja uliopita chini ya shinikizo kutoka kwa vuguvugu la maandamano makubwa lililotaka kuondolewa kwa siasa za kimadhehebu.Akizungumza baada ya kukutana na Rais Michel Aoun, Hariri alisema atautuma ujumbe kuzungumza na makundi makuu ya kisiasa, kuhakikisha kuwa yanautekeleza mpango wa Macron.

Ripoti: Taliban yamuidhinisha Trump katika uchaguzi wa rais

Rais wa Marekani Donald Trump amepata uungwaji mkono usiokuwa wa kawaida katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais na Novemba 3, baada ya kuidhinishwa na kundi la wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan. Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid ameiambia Televisheni ya Marekani ya CBS News katika mahojiano ya simu mwishoni mwa wiki kuwa wanatumai atashinda uchaguzi na kukamilisha mpango wa kuwaondoa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan. Lakini wanamgambo hao wa Taliban walielezea wasiwasi kuhusu Trump kuambukizwa ugonjwa wa COVID-19, wakisema walikuwa na wasiwasi na afya yake. Msemaji wa timu ya kampeni za Trump Tim Murtaugh siku ya Jumamosi alisema timu hiyo inakataa uungwaji mkono wa Taliban. Aliambia CBS News kuwa Taliban wanapaswa kufahamu kuwa rais wakati wote analinda maslahi ya Wamarekani kwa njia yoyote ile.

Matukio ya kisiasa

Matukio ya Afrika

Masuala ya jamii

Michezo

Habari kwa lugha ya Kiingereza

Redaktionsfoto Kisuaheli (DW/Joel Pawlak)

Bonyeza hapa kupata Matangazo na ripoti zetu

Matangazo
Tazama vidio 01:23