Svoboda | Graniru | BBC Russia | Golosameriki | Facebook
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo
Matangazo
Matangazo
HABARI

Habari za Ulimwengu | 28.06.2021 | 08:00

Misri, Jordan na Iraq kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi

Wakuu wa nchi za Misri, Jordan na Iraq wamefanya mkutano wa kilele jana Jumapili na kukubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi. Rais wa Misri Abdel Fatah al Sisi kwa mara ya kwanza alikwenda Iraq kushiriki mkutano huo pamoja na Mfalme Abdulla II wa Jordan na viongozi wa Iraq. Ziara hiyo imekuja wakati nchi hiyo ya Iraq ikitaka kujisogeza karibu kwa washirika wa Marekani wa nchi za Kiarabu katika Mashariki ya Kati. Iraq pia inataka kujionesha kama msuluhishi kati ya nchi za Kiarabu na Iran baada ya kuripotiwa kuandaa mazungumzo mwezi Aprili kati ya Iran na Saudi Arabia. Rais Al Sisi na Mfalme Abdallah II wa Jordan walikutana na wenyeji wao, Rais Barham Saleh na Waziri Mkuu Mustafa al Kadhemi, ambapo rais huyo wa Iraq alisema ujumbe uliotokana na mkutano wao ulikuwa muhimu katika wakati huu ambapo kuna changamoto nyingi za kikanda. Aidha viongozi hao walijadiliana kuhusu suluhisho la kisiasa linalozingatia azimio la Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Syria.

Kikosi cha Marekani chashambulia wanamgambo Iraq na Syria

Jeshi la Marekani chini ya maelekezo ya Rais Joe Biden limefanya mashambulizi dhidi ya kile kinachoitwa maeneo yanayotumiwa na makundi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran, karibu na mpaka baina ya Iraq na Syria. Katibu wa habari katika Wizara ya Ulinzi ya Marekani, John Kirby, amesema wanamgambo hao walikuwa wakitumia maeneo hayo kuendesha mashambulizi ya angani ya ndege zisizotumia rubani yakilenga magari ya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq. Kirby amesema kikosi cha wanajeshi wa Marekani kiliyalenga majengo matatu yanayotumiwa kuendesha mashambulio na kuweka silaha, mawili yakiwa Syria na moja nchini Iraq. Kwa mujibu wa katibu huyo wa habari katika wizara ya ulinzi ya Marekani, mashambulizi hayo ya anga yalikuwa ni ya kujilinda akisema yamefanywa kujibu mashambulizi ya makundi yanayoungwa mkono na Iran. Mashambulizi hayo ya Jumapili ni ya pili ya kijeshi chini ya utawala wa Rais Joe Biden katika ukanda huo.

Blinken na Lapid wakutana Rome

Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Israel jana walikutana mjini Rome, Italia, kwa mazungumzo wakati ambapo serikali mpya za nchi zao zikitarajia kufungua ukurasa mpya baada ya kuondoka viongozi wa zamani, Donald Trump na Benjamin Netanyahu. Wakiingia kwenye mazungumzo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Yair Lapid, amemwambia mwenzake wa Marekani, Antony Blinken, kwamba katika kipindi cha miaka michache iliyopita kuna makosa yaliyofanywa msimamo wa Israel wa kushirikiana na vyama viwili vinavyokinzana nchini Marekani haukuwa mzuri na hilo ni kosa wanaloweza kulirekebisha wote. Lapid amesema tangu alipochukua nafasi ya waziri wa mambo ya nje ameshazungumza na wanasiasa wa vyama Democrat na Republican na kuwakumbusha kwamba nchi yake Israel ina misingi sawa muhimu na Marekani ya uhuru, demokrasia, soko huru na kutafuta amani. Kwa upande wake, Blinken amezungumzia juu ya kuendelezwa usitishaji wa mapigano uliomaliza vita kati ya watawala wa Gaza na Israel pamoja na kutia msukumo juu ya kufufuliwa mazungumzo yaliyokwama ya kutafuta amani kati ya Israel na Palestina ambayo amesema yanaweza kuleta usawa.

Magari 28 ya wanajeshi wa UN Mali yaondolewa Gao

Magari yote yaliyoharibiwa kwenye mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Ujerumani katika kikosi cha walinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali yamekwishaondolewa katika eneo la tukio kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani. Annegret Kramp-Karrenbauer ameiambia Kamati ya Ulinzi ya Bunge la Ujerumani kwamba magari hayo 28 yaliyoharibiwa yamesharudishwa katika kambi ya Castor Field iliyoko nje ya mji wa Gao. Wanajeshi 12 wa Ujerumani walijeruhiwa kufuatia mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya kikosi hicho huko kaskazini mwa mji wa Gao. Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Jnim ndio wanaoendesha hujuma kwenye eneo hilo. Wanajeshi waliojeruhiwa walisafirishwa kuletwa Ujerumani na wanatibiwa katika hospitali za miji ya Ulm na Koblenz.

Mwandishi wa gazeti linalounga mkono demokrasia Hong Kong akamatwa

Mwandishi wa makala za maoni katika gazeti linalounga mkono demokrasia katika jimbo la Hong Kong la Apple Daily amekamatwa katika uwanja wa ndege jana usiku wakati akijaribu kuukimbia mji huo. Vyombo vya habari vya Hong Kong vimeripoti juu ya tukio hilo ambapo gazeti la South China Morning Post na kituo cha habari cha mtandao cha Citizen News vilitoa habari hiyo likinukuu vyanzo ambavyo havikutajwa. Kwa mujibu wa ripoti zao, mwandishi habari Fung Wai-Kong alikamatwa baada ya kushukiwa kuwa na njama na watu kutoka nje kuhatarisha usalama wa taifa. Inaaminika kwamba Fung alikuwa akielekea Uingereza wakati alipokamatwa.

Italy yaondowa uvaaji barakoa

Rome,Italia imeondowa uvaaji barakoa nchi nzima ambapo imetajwa kwamba kitisho ni kidogo, hatua ambayo ni kubwa katika nchi hiyo iliyokuwa ya kwanza kuathirika vibaya zaidi na virusi vya Corona barani Ulaya mnamo mwezi Februari mwaka 2020. Hatua hiyo imeanza kutekelezwa leo Jumatatu ambapo wizara ya afya nchini humo imesema mikoa yote 20 ya nchi ni salama na kwamba kitisho ni cha chini kwa mujibu wa utaratibu wa mfumo wa taifa wa kupima viwango vya kitisho cha Covid-19. Giovanni di Perri mkurugenzi wa hospitali ya magonjwa ya kuambukiza amesema maambukizo yamepungua sana nchini humo,sababu mojawapo ikiwa inatokana na watu wengi kuchanjwaHilo linamaanisha kwamba watu hawalazimiki kuvaa barakoa nchini humo ambako viwango vya joto vinatarajiwa kupanda kufikia nyuzi joto 40 wiki hii katika maeneo yake ya Kusini.

Ubelgiji yaingia robo fainali kwa kuwaliza Ureno

Timu ya taifa ya soka ya Ubelgiji ilitwaa ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya Ureno katika mchuano mkali hapo jana na kufanikiwa kuingia robo fainali ya Kombe la Mabingwa barani Ulaya-Euro-2020. Katika mchuano huo uliochezwa huko Seville, mchezaji Thorgen Hazard ndiye aliyeutikisa wavu wa timu ya Ureno kwa mkwaju mrefu uliokwenda kushoto kisha kurudi kulia na hatimae kukatiza mpaka ndani ya wavu na kuihakikishia ushindi timu hiyo katika mchuano wa mchujo wa timu 16. Mchezaji huyo kiungo anayecheza soka na klabu ya Ujerumani katika Bundesliga amesema kwa kutazama idadi ya maoni aliyopokea kwenye simu yake ya mkononi inaonesha goli lake la jana ndio goli muhimu zaidi tangu alipoanza kucheza soka.

MATUKIO YA KISIASA
MATUKIO YA AFRIKA
MASUALA YA JAMII
MICHEZO
HABARI KWA LUGHA YA KIINGEREZA

Matangazo
Tazama vidio 04:09

Vidio zaidi

Mfahamu Diyana Laizer, mwanzilishi wa Consumers Award

Mfahamu Diyana Laizer, mwanzilishi wa Consumers Award

Ukuzaji wa Filamu na Sanaa Uganda

Ukuzaji wa Filamu na Sanaa Uganda

Vazi la shingoni kwa wanawake wa Kimaasai

Vazi la shingoni kwa wanawake wa Kimaasai

Ujerumani yatinga 16 bora katika michuano ya Euro 2020

Ujerumani yatinga 16 bora katika michuano ya Euro 2020

Faida Musafiri, mjane wa Bukavu asiyekata tamaa

Faida Musafiri, mjane wa Bukavu asiyekata tamaa

TUFUATILIE KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII
MICHUANO YA MATAIFA YA ULAYA EURO 2020