Svoboda | Graniru | BBC Russia | Golosameriki | Facebook
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo
Matangazo
Matangazo
HABARI

Habari za Ulimwengu | 28.06.2021 | 13:00

Mkuu wa tume ya haki za binadamu ataka mifumo ya kibaguzi iondolewe duniani

Mkuu wa Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa leo ametowa mwito wa kumalizwa mara moja mifumo ya kibaguzi dhidi ya watu weusi kote duniani kuepusha kilichotokea katika mauaji ya Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika, George Floyd. Katika ripoti iliyochochewa na kifo cha Mmarekani huyo aliyeuwawa na polisi wa kizungu, Michelle Bachellet amesema ukandamizaji wa kuwabagua watu wenye asili ya Kiafrika umeondowa utamaduni wa kuvumiliana na badala yake kuchochea ubaguzi kwa misingi ya rangi pamoja na kuzusha machafuko. Mkuu huyo wa Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa ametangaza mpango wa ajenda nne kwa ajili ya kuleta mageuzi katika suala la kuleta haki na usawa kwenye masuala yanayohusu rangi na kuzitolea mwito serikali kuutekeleza mpango huo. Rais huyo wa zamani wa Chile amewasilisha ripoti yake ya kurasa 23 mbele ya Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa ambapo miongoni mwa mapendekezo aliyoyatowa ni kulipwa fidia waliopitia vitendo vya ubaguzi wa rangi pamoja na kuyafadhili makundi ya harakati za kupinga ubaguzi wa rangi kama lile la Black Lives Matter.

Blinken akutana na Papa Francis

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, amefanya mazungumzo leo na viongozi wa Vatican kuhusu hatua za kuushughulikia mgogoro nchini Venezuela wakati akiwa ziarani katika makao makuu hayo ya Kanisa Katoliki duniani. Blinken ni afisa wa kwanza wa ngazi za juu chini ya serikali ya Rais Joe Biden kukutana na Papa Francis katika kikao kilichofanyika faragha.Aidha Blinken alikutana pia na Kardinali Petro Parolin anayehusika na mambo ya nje ya taasisi hiyo ya kiimani, Vatican. na Askofu Mkuu Paul Gallagher anayehusika na masuala ya uhusiano wa nje wa kanisa hilo ambapo wamejadili kuanzia migogoro nchini Venezuela, Syria, Lebanon, Belarus na Ethiopia, kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani. Blinken amesisitiza uungaji mkono wa Marekani katika kurudisha demokrasia nchini Venezuela na nia yao ya kutaka kuwasaidia wananchi wa Venezuela kuijenga upya nchi yao. Kesho atakwenda kusini mwa Italia kushiriki mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za kundi la G20 utakaozungumzia hatua ya kuimarisha ushirikiano miongoni mwa mataifa kuhusu mabadiliko ya hatia nchi, afya na maendeleo.

Viongozi wakuu wa China na Urusi waongeza ushirikiano wa kirafiki na ujirani mwema

Viongozi wakuu wa China na Urusi wamekubaliana kurefusha rasimu ya makubaliano ya ujirani mwema na ushirikiano wa kirafiki. Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya China, Xinhua, hatua hiyo imefikiwa leo wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika mkutano wa kilele kwa njia ya vidio kati ya marais Xi Jinping na Vladmir Putin. Katika mkutano huo, Putin amesema rasimu hiyo ya makubaliano ya msingi ya kuungana mkono katika kulinda mshikamano wa madola yao na uthabiti katika maeneo yao ni muhimu sana katika ulimwengu wa sasa. Urusi inaiuzia China mafuta, gesi na mkaa wa mawe wakati nchi hiyo yenye idadi kubwa ya watu duniani ikiiuzia Urusi mashine na bidhaa nyingine. Nchi zote mbili mara nyingi husimamia maslahi sawa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Jeshi la Iraq lakosoa mashambulizi ya anga ya Marekani

Msemaji wa jeshi la Iraq amelaani mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani jana dhidi ya wanamgambo katika eneo la mpaka kati ya nchi hiyo ya Iraq na Syria. Msemaji huyo wa jeshi la Iraq, Yehia Rasool, amesema kitendo cha Marekani ni ukiukaji wa mamlaka ya nchi yake. Kauli ya ukosoaji ya Iraq ni ya nadra dhidi ya Marekani. Rasool aliandika ujumbe huo wa kuikosoa Marekani kwenye ukurasa wa Twitter baada ya mashambulizi ya Marekani kuua wapiganaji kiasi wanne wa kundi la kikosi cha wanamgambo wa Kishia wanaofungamana na Iran.

Jeshi la India lazuia kitisho cha shambulio Kashmir

Jeshi la India limesema limezuia kitisho kikubwa baada ya kuzizuwia ndege mbili zisizoendeshwa na rubani zilizokuwa zikiruka kwenye anga la eneo iliko kambi ya jeshi hilo katika jimbo la Kashmir. Tukio hilo limefanyika leo Jumatatu, siku moja baada ya ndege zisizokuwa na rubani zilizoshukiwa kubeba miripuko kutumiwa kushambulia kambi ya jeshi la anga katika eneo hilo linalozozaniwa kati ya India na Pakistan. Jeshi limesema wanajeshi walizigundua ndege mbili usiku wa manane zikiwa zinaruka katika anga la eneo la kambi ya kijeshi ya Kaluchak nje ya mji wa Jammu na kuchukua hatua ya haraka kuzilenga ndege hizo ambazo ziliondoka. Hakuna kundi la waasi lilitowa kauli yoyote kuhusu tukio hilo. Jimbo la Kashmir limegawika kati ya upande wa India na Pakistan na kila upande unadai liko chini ya himaya yake.

Mpinzani wa Lukashenko akanusha mashtaka ya uhalifu yanayomkabili

Aliyewahi kuwa mtaalamu katika masuala ya benki na mpinzani maarufu nchini Belarus, Viktor Babariko, amekanusha mashtaka yote yanayomkabili katika kikao cha kusikiliza kesi yake mahakamani kilichofanyika leo. Babariko mwenye umri wa miaka 57 amesema hawezi kukiri kuhusika na uhalifu ambao hajaufanya na kuongeza kusema kwamba haoni fedheha kwa sababu hakuna kitendo cha uvunjaji sheria kilichotokea. Waendesha mashtaka wametaka afungwe miaka 15 jela. Babariko anatuhumiwa kuhusika na utakatishaji fedha, kutoa rushwa na kukwepa kulipa kodi. Mahakama inatarajiwa kutoa hukumu wiki ijayo. Babariko ambaye alikuwa mtaalamu wa masuala ya benki na mtu tajiri alikuwa miongoni mwa wapinzani wa Rais Alexender Lukashenko waliotiwa jela kabla ya uchaguzi wa rais Agosti 9. Alikamatwa akiwa na mwanawe wa kiume akielekea kwenye tume ya uchaguzi kutia saini fomu yake ya kugombea urais. Kukamatwa kwake kulikuja baada ya Rais Lukashenko kuamrisha msako katika benki aliyokuwa akiiongoza ya Belgazprom ambayo ni benki ya ukopeshaji ya tawi la kampuni ya gesi inayomilikiwa na Urusi ya Gazprom.

Chama tawala cha Kikomunisti China chajiandaa kusherehekea miaka 100

Chama tawala cha Kikomunisti cha China kinaadhimisha miaka 100 tangu kuundwa kwake kwa kuonesha kile ambacho inasema ni kuongezeka ushawishi wake nchi za nje pamoja na mafanikio katika kupambana na ufisadi na rushwa nchini humo. Maafisa wa chama hicho leo walimmiminia sifa Rais Xi Xinping ambaye amejionesha kuwa kiongozi mwenye nguvu zaidi tangu utawala wa Mao Zedong na ameondowa ukomo wa mihula ya kukaa madarakani. Naibu kiongozi wa idara ya mawasiliano ya ndani ya chama hicho, Guo Yezhou, amesema mbele ya waandishi habari katika ufunguzi wa kituo cha mikutano ya waandishi habari watakaoripoti sherehe hizo, kwamba ushawishi wa chama chao katika jukwaa la kimataifa, na mvuto wake umeendelea kuongezeka na kukifanya kuwa katika nafasi ya mbele katika siasa za ulimwengu. Sherehe za miaka 100 ya chama hicho itafanyika siku ya Alhamisi wiki hii.

Misri, Jordan na Iraq kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi

Wakuu wa nchi za Misri, Jordan na Iraq wamefanya mkutano wa kilele jana Jumapili na kukubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi. Rais wa Misri Abdel Fatah al Sisi kwa mara ya kwanza alikwenda Iraq kushiriki mkutano huo pamoja na Mfalme Abdulla II wa Jordan na viongozi wa Iraq. Ziara hiyo imekuja wakati nchi hiyo ya Iraq ikitaka kujisogeza karibu kwa washirika wa Marekani wa nchi za Kiarabu katika Mashariki ya Kati. Iraq pia inataka kujionesha kama msuluhishi kati ya nchi za Kiarabu na Iran baada ya kuripotiwa kuandaa mazungumzo mwezi Aprili kati ya Iran na Saudi Arabia.Rais Al Sisi na Mfalme Abdallah II wa Jordan walikutana na wenyeji wao, Rais Barham Saleh na Waziri Mkuu Mustafa al Kadhemi, ambapo rais huyo wa Iraq alisema ujumbe uliotokana na mkutano wao ulikuwa muhimu katika wakati huu ambapo kuna changamoto nyingi za kikanda. Aidha viongozi hao walijadiliana kuhusu suluhisho la kisiasa linalozingatia azimio la Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Syria.

MATUKIO YA KISIASA
MATUKIO YA AFRIKA
MASUALA YA JAMII
MICHEZO
HABARI KWA LUGHA YA KIINGEREZA

Matangazo
Tazama vidio 04:09

Vidio zaidi

Mfahamu Diyana Laizer, mwanzilishi wa Consumers Award

Mfahamu Diyana Laizer, mwanzilishi wa Consumers Award

Ukuzaji wa Filamu na Sanaa Uganda

Ukuzaji wa Filamu na Sanaa Uganda

Vazi la shingoni kwa wanawake wa Kimaasai

Vazi la shingoni kwa wanawake wa Kimaasai

Ujerumani yatinga 16 bora katika michuano ya Euro 2020

Ujerumani yatinga 16 bora katika michuano ya Euro 2020

Faida Musafiri, mjane wa Bukavu asiyekata tamaa

Faida Musafiri, mjane wa Bukavu asiyekata tamaa

TUFUATILIE KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII
MICHUANO YA MATAIFA YA ULAYA EURO 2020