Svoboda | Graniru | BBC Russia | Golosameriki | Facebook

Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Aprili 28, 2024 Local time: 00:23

UN: Wanawake na wasichana walio na ulemavu bado wakabiliwa na dhulma za kijinsia


Debora Nzisa, Mwanaharakati dhidi ya dhulma ya kijinsia, Mombasa, Kenya
Debora Nzisa, Mwanaharakati dhidi ya dhulma ya kijinsia, Mombasa, Kenya

Kulingana na Shirika la Kimataifa la UN Women,  wanawake na wasichana walio na ulemavu wanakabiliwa na dhulma za kijinsia  mara tatu zaidi ya wenzao wasio na ulemavu.

Wao hupata dhulma hizo kutoka kwa familia, shule, wanaowashughulikia, yaani ‘caregivers’ na hata katika vituo vya afya ama shule.

Ili kuwasaidia wanawake na wasichana, mwanamke mmoja huko katika pwani ya Mombasa nchini Kenya anaendeleza kampeni ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wenzake wanaoishi na ulemavu.

Mwanamke huyo ni Debora Nzisa mwenye umri wa maika 34 ambaye anaishi katika kitongoji cha Mishomoroni, Mombasa. Deborah ni mlemavu kutokana na ugonjwa wa Spina Bifida, hali iliyogundulika akiwa mtoto mchanga.

Kama ilivyo kwa wanawake walio na ulemavu, Debora anasimulia kuwa akiwa shuleni alitengwa na kubaguliwa.

Baada ya Kumaliza Masomo

Baada ya kumaliza masomo yake chuoni , alijiunga na shirika ambalo lengo lake kuu ni kuwawezesha vijana walio na ulemavu kuhusu haki zao msingi.

“Nilikuwa nawasaidia vijana wengine ambao wanakua bado, hadi sasa wale vijana wote wanakuwa wameapitia ubaguzi shuleni, tunaonana na wao tukienda kliniki nawasaidia na kuwashauri na kuwapa moyo na kuwaelekeza vipi wanaweza kuishi na jamii hata kama watabaguliwa wajue namna ya kuishi nao,” anasema Debora.

Dhulma za Kimapenzi

Debora jinsi alivyopitia dhulma za kimapenzi na kujitumbukiza katika mahusiano na mtu aliyedhani anampenda.

Ni kutokana na hali hiyo alijikuta akijitosa katika kampeni ya kupambana na dhulma za kijinsia hasa kwa wanawake wenzake walio na matatizo kama yake.

“Sasa nililinyamazia hilo, hadi nilipofika umri wa miaka 25 ndio nikafunguka kwa kaka yangu, jambo jengine baadhi ya marafiki zangu wanaoishi na ulemavu, walio katika ndoa wengine wanapitia ukatili wa kijinsia, wengine wanapitia ubaguzi na wakiwa hapo katika ndoa, hata inafika wakati wanaletewa mabibi wengine hapo hapo, wanapata kiwewe na hawezi kuongea. Akipata nafasi akiniambia mimi nampa ushauri asinyamaze,” anaongezea Debora.

Debora ni Msanii wa Nyimbo

Debora ambaye pia ni msanii wa nyimbo za injili alitumia kipaji chake kutunga wimbo wa kupiga vita dhulma za kijinsia.

Mbali na nyimbo pia hujiunga katika makundi ya vijana wanaoishi na ulemavu , kuwazungumzia kuhusu haki zao msingi.

Mwanaharati huyo wa kampeni dhidi ya ukatili wa kijinsia aelezea kuwa changamoto kubwa miongoni mwao ni kunyamaza wanapotendewa dhulma .

Hata hivyo vikao vyao vinazaa matunda kwani wengi wanazungumzia madhila wanayopitia.

Debora anaongezea, “tukikaa kama vijana tukiongea, tunakua huru na utapata mmoja anafunguka kama nimepata mchumba, na tukimuuliza maswali, anasema kuna siku ilikuwa hivi na hivi nikimuuliza na je ulimzungumzia anasema nilijaribu lakini hakuchukulia poa, kwa hiyo inakua sehemu salama kwa vijana kuzungumza na hapo tunasaidiana na ni vile tunasema kinachozungumzwa hapo hakifai kutoka nje, kwa hiyo tunafunguka.”

Mahusiano ya Kimapenzi

Je, kutokana na kile ulikipitia kwa sasa uko kwa mahusiano ama hutamani tena? “Kwa kweli kwa sasa nimejipa pumziko na kwamba kabla niamue kuolewa inabidi nikae nijielewe na nijue nini ninataka.”

Na huku serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yakiendelea na mikakati ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia miongoni mwa wanaoishi na ulemavu , Debora ambaye kwa sasa anasema hayumo katika mahusiano kutokana na yale aliyopitia, hivyo ana ushauri huu kwa wenzake.

“ Nawahimiza wanaoishi na ulemavu wanawake hata wanaume pia wanaathirika na GBV na wale wengine hawana ulemavu wasinyamaze wakiona wanateswa katika ndoa, wakiona wanateswa kiakili katika ndoa wanafaa kuzungumza ili wapate msaada, hayo mashirika ya GBV yana namba hutoa kwa hiyo wapige hizo namba wapewe msaada unaostahili.”

Imeatayarishwa na mwandishi wetu Amina Chombo,VOA Mombasa.

Forum

XS
SM
MD
LG