Svoboda | Graniru | BBC Russia | Golosameriki | Facebook

Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Aprili 29, 2024 Local time: 16:08

KENYATTA: Nilikuwa tayari kuachia wapinzani wangu madaraka ili kuepusha umwagikaji wa damu mwaka 2017


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema kwamba alikuwa tayari kuachia madaraka baada ya mahakama kuu kufutilia mbali ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, ili kuzuia umwagikaji wa damu lakini naibu wake alimshawishi kutofanya hivyo.

Hii ni mara ya kwanza Uhuru amezungumzia yaliyokuwa yakiendelea katika fikra zake, baada ya mahakama kuu kufuta ushindi wake na kuagiza marudio ya uchaguzi huo kufuatia kesi ya kupinga matokeo ya kura, iliyowasilishwa katika mahakama hiyo na Raila Odinga na muungano wake wa kisiasa wa NASA.

Uhuru amesema hayo Ijumaa (Julai 8 2022) wakati wa mkutano na viongozi wa kidini kutoka jamii ya wakikuyu, uliofanyika katika ikulu ya rais, Nairobi.

“Nilikuwa tayari kuachia madaraka, kuweka maslahi ya nchi mbele na kuokoa nchi dhidi ya umwagikaji wa damu.” Amesema uhuru katika hotuba aliyotoa akitumia lugha ya kikuyu, akiongezea kwamba “haya madaraka tuliyo nayo hayana thamani sana kushinda maisha ya watu. Ndio! Nilikuwa nimeamua kuachia madaraka na kuokoa nchi.”

Ujumbe wa sauti ya Ruto kwamba alikuwa anataka kumpiga kofi Uhuru

Uhuru alikuwa akizungumzia ujumbe wa sauti ambao umekuwa ukisambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo naibu rais Dr. William Ruto anasikika akisema kwa kejeli kwamba alikuwa karibu kumzaba kofi rais Uhuru Kenyatta baada ya mahakama kuu kufutilia mbali ushindi wao.

“Mimi nikatoka hapo, nikafika State House. Kufika statehouse nikapata rafiki yangu yuko hapo. Sitaki kusema alikuwa anafanya nini kwa sababu sisi ni wazee…. Ndiye huyo ehh…mmhh..sasa, hiyo maneno… sijui nini…. Mimi sitaki… mimi nataka kwenda Ichaweri…ehhh… wewe.. sijui sasa wacha tuachane na hii kitu. Mimi nikamwangaliaaaa…… nikamwambia weweee… ni vile tu nilikuwa na heshima. Ningemchapa kofi. Ati sisi tuwache … ati tutoke hapa…. Ahhh hapanaaa..hapana!” Inasikika sauti ya Ruto yenye kicheko ndani na inayosikika kama iliyojaa utani ndani yake huku watu waliokuwa wakimsikiliza pia wakicheka. Haijulikani mahali ujumbe huo ulirekodiwa wala siku.

Wapinzani wa Ruto wametumia ujumbe uliorekodiwa katika kampeni dhidi yake

Sauti hiyo, imetumika katika mikutano ya kisiasa nchini Kenya, wapinzani wakisema kwamba Ruto alitaka kumpiga kofi rais Kenyatta, ishara ya kutomheshimu rais.

Na baada ya siku kadhaa za ujumbe huo wa sauti kusambaa kwa mitandao ya kijamii na kuchezwa kwenye mikutano ya siasa, Kenyatta amevunja ukimya na kusema, “iwapo wangenipiga kofi kwa sababu ya madaraka, ningewapa shavu la pili na wapige kofi lingine. Ndio, nilitaka kuachia madaraka na niende Ichaweri kwa sababu nisingeweza kulinganisha madaraka na umwagikagi wa damu.”

Ichaweri ni kijijini kwa Uhuru Kenyatta. Kinapatikana eneo bunge la Gatundu kusini, Kaunti ya Kiambu, kilomita 50 kutoka Nairobi.

Ruto ametetea ujumbe huo

Ruto ametetea ujumbe huo wa sauti akisema kwamba hakuna vile angemruhusu rais Kenyatta kuacha madaraka kwa upinzani ulioongozwa na Raila Odinga.

“Uhuru alikuwa ameanza kuonyesha dalili za kukata tamaa. Aliniambia kwamba alikuwa anataka kuacha urais na kwenda kijijini kwake, Ichaweri. Hata kama nilimlazimisha Uhuru kuwa rais, kuna shida gani? Wafuasi wa Azimio wanastahili kuacha huu upuuzi. Wanasambaza ujumbe uliorekodiwa wakisema kwamba Ruto alimlazimisha Uhuru kuwa rais. Kama ingekuwa wewe, ungeruhusu Uhuru atuache na vile tulikuwa tumemsukuma?” alieleza Ruto katika mkutano wa kisiasa.

Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula, wakiwa katika muungano wa NASA, walielekea mahakamani mwaka 2017 kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais.

Mahakama ya juu zaidi ya Kenya ilikubali hoja zilizowasilishwa na muungano wa NASA na kuagiza tume huru ya uchaguzi IEBC kuandaa upya uchaguzi wa urais.

Odinga ajiondoa kwenye marudio ya uchaguzi na kuitisha maandamano

Raila Odinga alijiondoa katika marudio ya uchaguzi huo na kuamua kuandaa maandamano akitaka makamishna wa tume huru ya uchaguzi IEBC kuondoka ofisini.

Hali ya wasiwasi iliongezeka Kenya. Raila alijiapisha kama rais, na ghasia zikaripotiwa katika baadhi ya sehemu za Kenya.

Katika kikao cha Ijumaa katika ikulu ya rais, uhuru vile vile amesema kwamba aliamurisha maafisa wa usalama kutopelekwa katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi ambako Raila Odinga alikuwa anajiapisha. Amesema kwamba wanajeshi walikuwa wamepangiwa kushika doria katika uwanja huo na kumzuia Raila kujiapisha.

‘Wakati mambo yalikuwa mabaya, kuna watu walikuwa wanataka kujiapisha, kuna wale walioniambia kwamba nitume wanajeshi kukabiliana na waliokuwa wanajiapisha lakini nilikataa kabisa.” Amesema Uhuru.

Miguna Miguna aliongoza kuapishwa kwa Raila

Raila alijiapisha kama rais mnamo Januari 30, 2018 baada ya maandamano ya siku kadhaa.

Shughuli ya kujiapisha iliongozwa na Miguna Miguna ambaye alikuwa kama jaji wake mkuu, akisaidiwa na wakili TJ Kajwang.

Matangazo yote ya televisheni na radio yalizimwa wakati wa sherehe hiyo ya kuapishwa iliyochukua muda wa dakika moja na sekunde 15. Mitandao ya kijamii ilizimwa.

Moses Wetangula, Musalia Mudavadi na Kalonzo Musyoka ambao walikuwa vinara wakuu wa muungano wa NASA hawakuhudhuria shughuli ya Raila kujiapisha.

Baadaye Miguna Miguna alifurushwa kutoka nchini Kenya na sasa yupo Canada. Amejaribu kurudi Kenya bila mafanikio. Kila ndege imepewa ilani na hakuna ndege inayoingia Kenya inaruhusiwa kumbeba Miguna Miguna.

Moses Wetangula na Musalia Mudavadi walimtoroka Odinga na sasa wamejiunga na William Ruto.

Kalonzo Musyoka alikuwa amemtoroka Odinga lakini akarudi katika muungano wa Azimio, wake Odinga japo kwa kunung'unika akidai ametengwa na kunyimwa nafasi ya kuwa mgombea mwenza. Muungano wa NASA ulisambaratika.

Handshake kati ya Uhuru na Raila

Machi 9, 2018, rais Uhuru Kenyatta alifanya mazungumzo na Raila Odinga na kufikia makubaliano yanayojulikana sana Kenya kama handshake na kutuliza joto la kisiasa.

Tangu wakati huo, Raila amekuwa akishirikiana na Kenyatta katika kuiongoza Kenya, akisema jukumu lake limekuwa kumshauri rais Kenyatta.

Naibu rais Dr. William Ruto na wafuasi wake hata hivyo wamekuwa wakikosoa ushirikiano wa Raila na Uhuru Kenyatta tangu wakati huo, wakisema kwamba umelemaza malengo ya maendeleo ya serikali ya Jubilee.

Kuvunjika kwa chama cha Kenyatta cha Jubilee

Chama cha Uhuru Kenyatta cha Jubilee kilivunjika baada yake kuingia ushirikiano na Raila, na kuunda vyama vingine vya kisiasa ikiwemo chama cha Ruto cha United democratic Alliance UDA na muungano wa Kenya Kwanza ambao Ruto anatumia kugombea urais katika uchaguzi wa mwezi ujao wa Agosti.

Rais Uhuru Kenyatta anamuunga mkono Raila Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua katika uchaguzi huo. Uhuru amefichua kwamba ndiye aliyemchagua Martha Karua kuwa mgombea mwenza wa Raila.

“Licha ya ukweli kwamba sijawahi kusikilizana na Martha kisiasa, ni mtu mwenye msimamo. Ni heri kufuata mtu ambaye ni mkweli, mpenda haki na mwenye kiu ya kuwatumikia watu na sio ubinafsi,” amesema Uhuru.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG