Svoboda | Graniru | BBC Russia | Golosameriki | Facebook

Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Aprili 29, 2024 Local time: 09:01

Wataalamu wahimiza watoto wafundishwe lugha za asili


Wanafunzi wa shule ya msingi ya Msomera , Handeni wakiwa darasani July 15, 2022. Picha na AFP
Wanafunzi wa shule ya msingi ya Msomera , Handeni wakiwa darasani July 15, 2022. Picha na AFP

Lugha ya Mama au lugha ya asili ni msingi imara wa kujifunza lugha nyingine. Kwasababu ni lugha ya kwanza ambayo mototo anajifunza nyumbani kabla ya kuanza masomo.

Wataalamu na wadau wa lugha ya Kiswahili nchini Tanzani na Kenya wamesema lugha za asili ni muhimu kwa watoto wafundishwe kabla ya kuanza masomo ili kuikuza lugha ya Kiswahili yenye maingiliano na lugha hizo za asili za Kiafrika.

Profesa Edward Oyugi, mmoja wa wataalam wa lugha za asili Kenya, anasema kuwa wakati umefika kwa lugha ya mama kuhimizwa katika mazungumzo na jamii katika bara la Afrika lenye lugha zaidi ya elfu mbili.

Nchini Tanzania Wataalamu na wadau hao wa Kiswahili , wamehimiza umuhimu wa kuhifadhi lugha hizo za asili kwa kuandika vitabu na kamusi ikiwa ni urithisha wa lugha za asili kwa vizazi vijavyo.

Matamshi ya profesa Oyugi, yametolewa siku moja baada ya kuadhimishwa Siku ya Kimataifa ya lugha ya Mama ili kusaidia kuimarisha utamaduni wa makabila mbali mbali.

Waatalamu wanasema kuandika vitabu na kamusi za lugha hizo ni njia muhimu ya kuhamisha maarifa kwa vizazi vijavyo na kukuza lugha ya asili, kwani pole pole lugha hizo zitakuwa kwenye hatari ya kutoweka.

Aidha wamesema vitabu vinaweza kuwa vyanzo imara vya kujifunza na kufundisha, na pia vinaweza kuchangia katika kuimarisha matumizi na ustawi wa lugha.

Dkt. Seleman Sewanji, ametoa wito kwa jamii kushiriki katika juhudi hizo. Akisisitiza umuhimu wa kila mtu aliye na ujuzi wa lugha yake kuandika kamusi au tamaduni zinazohusiana na lugha hizo. Kwa kufanya hivyo, wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha na kukuza lugha ya Kiswahili.

Wanafunzi wa shule ya msingi iliyoko katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Miracle and Victory huko Kibera Nairobi.
Wanafunzi wa shule ya msingi iliyoko katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Miracle and Victory huko Kibera Nairobi.

"Ninatoa wito kwa jamii kwamba kama kuna mtu mwenye uwezo wa kuandika kamusi ya lugha yake au tamaduni zinazohusiana na lugha hiyo, aichapishe na kuiweka wazi. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kurutubisha lugha yetu ya Kiswahili," amesisitiza Sewanji.

Tanzania inakadiriwa kuwa na na karibu lugha za asili 120 na Kenya zaidi ya sitini. Kingereza na Kiswahili zikiwa lugha rasmi za taifa.

Wasomi wanaeleza wasi wasi kutokana na uwezekano wa kupotea kwa lugha hizo kutokana na athari za utandawazi, ongezeko la mawasiliano ya kimataifa, teknolojia, na mabadiliko ya kijamii yamechochea watu kuhamia kutumia lugha za kigeni, hasa katika mazingira ya mijini

Dkt. Mwanahija Ali, Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Zanzibar, amesema kutoweka kwa lugha mama katika jamii kutaletea athari kubwa kwa vizazi vijavyo kutokufahamu utamaduni wao kwani ndani ya lugha mama kuna utamaduni wa kutosha.

“Kwa hiyo, kama itapotea lugha mama, utapotea utamaduni kwani ndani ya lugha mama kuna utamaduni wa kila aina, kama vile utamaduni wa mavazi na utamaduni wa chakula."

Kulingana na katiba ya Kenya, serikali ina jukumu la kuimarisha lugha ya mama katika makabila yote nchini. Profesa Oyugi, anaeleza ni kwanini wakati umefika kwa lugha ya mama barani Afrika inafaa kuhimizwa katika mazungumzo na jamii.

"Kudumisha uzungumzaji wa lugha ya mama barani Afrika ni muhimu kwa kuhifadhi kikamilifu kwa lugha hizo. Lugha ya mama inatambua haraka jamii inayoizungumza. Bara la Afrika lina utajiri mkubwa wa uzungumzaji wa lugha ya mama, ikitiliwa maanani kuwa Afrika ina lugha zaidi ya elfu-mbili. Bahati mbaya nyingi za lugha hii ya mama zinakaribia kudidimia kabisa kwa sababu uigizaji wa lugha za kigeni duniani. Uigizaji huo umechangia kwa sehemu kubwa katika kutoweka lugha ya mama barani Afrika," Profesa Oyugi.

Kwa kusisitiza elimu kupitia lugha nyingi, jamii inaweza kuimarisha mchakato wa kujifundisha na kuhakikisha urithi wa maarifa na utamaduni unapewa vizazi vijavyo.

Hii ripoti imetayarishwa Amri Ramadhani, Tanzania na James Shimanyula, Kenya.

Forum

XS
SM
MD
LG